Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:22-35

Ezekieli 23:22-35 NEN

“Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande: Wababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi. Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kofia za chuma. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao. Nitaelekeza wivu wa hasira yangu dhidi yako, nao watakushughulikia kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako na binti zako, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto. Watakuvua pia nguo zako na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu. Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani tena, wala kukumbuka Misri tena. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia. Watakushughulikia kwa chuki na kukunyangʼanya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako, kikombe kikubwa na chenye kina kirefu; nitaletea juu yako dharau na dhihaka, kwa kuwa kimejaa sana. Utalewa ulevi na kujawa huzuni, kikombe cha maangamizo na ukiwa, kikombe cha dada yako Samaria. Utakinywa chote na kukimaliza; utakivunja vipande vipande na kuyararua matiti yako. Nimenena haya, asema BWANA Mwenyezi. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”