Kutoka 4:1-17
Kutoka 4:1-17 BHN
Mose akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Unashika nini mkononi mwako?” Mose akamwambia, “Fimbo.” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Mose akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Mose akaikimbia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Mose akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.” Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Mose akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji. Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Mose akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake. Mungu akamwambia Mose, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili. Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Ewe Bwana wangu, mimi sina ufasaha wa kuongea tangu zamani; hata baada ya wewe kusema nami mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu? Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi? Aone au awe kipofu? Je, si mimi Mwenyezi-Mungu? Basi, nenda! Mimi nitakiongoza kinywa chako na kukufundisha cha kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana wangu, tafadhali nakusihi, umtume mtu mwingine.” Ndipo hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Je, si yuko ndugu yako Aroni ambaye ni Mlawi? Najua yeye ana ufasaha wa kuongea. Tena anakuja kukutana nawe, na mara tu atakapokuona atafurahi moyoni. Wewe utaongea naye na kumwambia yote atakayosema. Mimi nitawasaidieni na kuwafundisha mambo mtakayofanya. Aroni ataongea na Waisraeli kwa niaba yako. Yeye atakuwa msemaji wako, nawe utakuwa kama Mungu kwake. Utaichukua mkononi mwako fimbo hii ambayo utaitumia kufanya zile ishara.”