Kutoka 4:1-17
Kutoka 4:1-17 NEN
Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘BWANA hakukutokea’?” Ndipo BWANA akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akajibu, “Fimbo.” BWANA akasema, “Itupe chini.” Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. Kisha BWANA akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. BWANA akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa BWANA, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.” Kisha BWANA akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake. Ndipo BWANA akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.” Mose akamwambia BWANA, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.” BWANA akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, BWANA? Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.” Ndipo hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Aroni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. Aroni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”