Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 4:1-17

Kutoka 4:1-17 SRUV

Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia kutoka mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, nenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.

Soma Kutoka 4

Video ya Kutoka 4:1-17