Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 4:1-17

Kutoka 4:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mose akamwambia Mungu, “Lakini Waisraeli hawataniamini wala kunisikiliza, bali watasema kuwa wewe Mwenyezi-Mungu hukunitokea.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Unashika nini mkononi mwako?” Mose akamwambia, “Fimbo.” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Itupe chini.” Mose akaitupa fimbo chini, nayo ikageuka kuwa nyoka! Mose akaikimbia. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako, umkamate mkia!” Mose akanyosha mkono wake, akamkamata; nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Hivyo Waisraeli watapata kuamini kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, nimekutokea.” Tena, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Ingiza mkono wako kifuani mwako.” Mose akafanya hivyo, lakini alipoutoa nje, kumbe ukawa na ukoma; mweupe kama theluji. Kisha Mungu akamwambia, “Ingiza tena mkono wako kifuani mwako!” Mose akauingiza mkono wake kifuani. Na alipoutoa nje, kumbe ukarudia hali yake ya kawaida kama ulivyo mwili wake. Mungu akamwambia Mose, “Wasipokuamini au kusadiki ishara ya kwanza, yawezekana wakaamini ishara ya pili. Lakini wasipoamini hata ishara hizi mbili, au kuamini maneno yako, utachota maji ya mto Nili na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Maji hayo yatakuwa damu juu ya nchi kavu.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Ewe Bwana wangu, mimi sina ufasaha wa kuongea tangu zamani; hata baada ya wewe kusema nami mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito.” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyeumba kinywa cha mtu? Ni nani amfanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi? Aone au awe kipofu? Je, si mimi Mwenyezi-Mungu? Basi, nenda! Mimi nitakiongoza kinywa chako na kukufundisha cha kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana wangu, tafadhali nakusihi, umtume mtu mwingine.” Ndipo hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Je, si yuko ndugu yako Aroni ambaye ni Mlawi? Najua yeye ana ufasaha wa kuongea. Tena anakuja kukutana nawe, na mara tu atakapokuona atafurahi moyoni. Wewe utaongea naye na kumwambia yote atakayosema. Mimi nitawasaidieni na kuwafundisha mambo mtakayofanya. Aroni ataongea na Waisraeli kwa niaba yako. Yeye atakuwa msemaji wako, nawe utakuwa kama Mungu kwake. Utaichukua mkononi mwako fimbo hii ambayo utaitumia kufanya zile ishara.”

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia kutoka mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, nenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.

Shirikisha
Soma Kutoka 4

Kutoka 4:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘BWANA hakukutokea’?” Ndipo BWANA akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?” Akajibu, “Fimbo.” BWANA akasema, “Itupe chini.” Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. Kisha BWANA akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. BWANA akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa BWANA, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.” Kisha BWANA akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji. Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake. Ndipo BWANA akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili. Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.” Mose akamwambia BWANA, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.” BWANA akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, BWANA? Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.” Ndipo hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Aroni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. Aroni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”

Shirikisha
Soma Kutoka 4