Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mhubiri 2:1-11

Mhubiri 2:1-11 BHN

Basi, nikawaza; “Ngoja nijitumbukize katika starehe, nijifurahishe.” Lakini, niligundua kwamba kufanya hivyo ni bure kabisa. Nikasema kuhusu kicheko, “Ni wazimu”, na starehe “Mna faida gani?” Nilifikiria sana, namna ya kujichangamsha akili kwa divai, huku nikisukumwa na ari yangu ya kupata hekima; pia namna ya kuandamana na upumbavu ili nione yaliyo bora kabisa ambayo wanadamu wanaweza wakafanya waishipo maisha yao mafupi hapa duniani. Nilifanya mambo makuu: Nilijenga majumba na kujilimia mashamba ya mizabibu. Nilijifanyia bustani na viunga, nikapanda miti ya matunda ya kila aina. Nilijichimbia mabwawa ya maji ya kumwagilia hiyo miti. Nilinunua watumwa, wanawake kwa wanaume, na wengine wakazaliwa nyumbani mwangu. Nilikuwa na mali nyingi, makundi ya ng'ombe na kondoo wengi kuliko mtu yeyote aliyenitangulia kukaa Yerusalemu. Nilijirundikia fedha na dhahabu kutoka hazina za wafalme na toka mikoani, nami nilipata waimbaji wanaume kwa wanawake, na masuria watamaniwao. Naam, nikawa mkuu, mkuu kuwapita wote waliopata kuwako Yerusalemu kabla yangu; na hekima yangu ikakaa ndani mwangu. Kila macho yangu yalichokitamani nilikipata. Moyo wangu sikuunyima raha yoyote ile; kwa kuwa moyo wangu ulifurahia niliyotenda, na hili lilikuwa tuzo la jasho langu. Kisha nikafikiria yote niliyokuwa nimefanya kwa mikono yangu, jinsi nilivyotoa jasho katika kufanya hayo. Nikagundua kwamba yote yalikuwa bure kabisa; ilikuwa ni sawa na kufukuza upepo, hapakuwapo faida yoyote chini ya mbingu.

Soma Mhubiri 2