Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mhubiri 2:1-11

Mhubiri 2:1-11 NEN

Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu. Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima. Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote. Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.