Mhubiri 2:1-11
Mhubiri 2:1-11 SRUV
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ungali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyia mambo makuu; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyia mabwawa ya maji, ya kuunyweshea msitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kuliko wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, wanaume kwa wanawake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo. Wala sikuyanyima macho yangu chochote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yoyote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kufukuza upepo, wala faida hakuna chini ya jua.