Mhubiri 2:1-11
Mhubiri 2:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo. Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
Mhubiri 2:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nikawaza; “Ngoja nijitumbukize katika starehe, nijifurahishe.” Lakini, niligundua kwamba kufanya hivyo ni bure kabisa. Nikasema kuhusu kicheko, “Ni wazimu”, na starehe “Mna faida gani?” Nilifikiria sana, namna ya kujichangamsha akili kwa divai, huku nikisukumwa na ari yangu ya kupata hekima; pia namna ya kuandamana na upumbavu ili nione yaliyo bora kabisa ambayo wanadamu wanaweza wakafanya waishipo maisha yao mafupi hapa duniani. Nilifanya mambo makuu: Nilijenga majumba na kujilimia mashamba ya mizabibu. Nilijifanyia bustani na viunga, nikapanda miti ya matunda ya kila aina. Nilijichimbia mabwawa ya maji ya kumwagilia hiyo miti. Nilinunua watumwa, wanawake kwa wanaume, na wengine wakazaliwa nyumbani mwangu. Nilikuwa na mali nyingi, makundi ya ng'ombe na kondoo wengi kuliko mtu yeyote aliyenitangulia kukaa Yerusalemu. Nilijirundikia fedha na dhahabu kutoka hazina za wafalme na toka mikoani, nami nilipata waimbaji wanaume kwa wanawake, na masuria watamaniwao. Naam, nikawa mkuu, mkuu kuwapita wote waliopata kuwako Yerusalemu kabla yangu; na hekima yangu ikakaa ndani mwangu. Kila macho yangu yalichokitamani nilikipata. Moyo wangu sikuunyima raha yoyote ile; kwa kuwa moyo wangu ulifurahia niliyotenda, na hili lilikuwa tuzo la jasho langu. Kisha nikafikiria yote niliyokuwa nimefanya kwa mikono yangu, jinsi nilivyotoa jasho katika kufanya hayo. Nikagundua kwamba yote yalikuwa bure kabisa; ilikuwa ni sawa na kufukuza upepo, hapakuwapo faida yoyote chini ya mbingu.
Mhubiri 2:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ungali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyia mambo makuu; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyia mabwawa ya maji, ya kuunyweshea msitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kuliko wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, wanaume kwa wanawake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo. Wala sikuyanyima macho yangu chochote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yoyote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kufukuza upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
Mhubiri 2:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu. Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike na watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima. Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa ambayo niliunyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote. Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua.