Zaburi 69:1-15
Zaburi 69:1-15 SRUV
Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha. Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofika Kwa kumngoja Mungu wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali ni wengi, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nililipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua. Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu. Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli. Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na asiyetambuliwa na wana wa mama yangu. Maana mvuto wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata. Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Nikalaumiwa kwa hayo. Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa kifani cha dharau kwao. Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki. Nami maombi yangu nakuomba Wewe, BWANA, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako. Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe kutoka kwa wanaonichukia, Na kutoka katika vilindi vya maji. Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala Shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.