Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 69:1-15

Zaburi 69:1-15 NEN

Ee Mungu, niokoe, kwa maana maji yamenifika shingoni. Ninazama kwenye vilindi vya matope, pasipo mahali pa kukanyaga, Nimefika kwenye maji makuu, mafuriko yamenigharikisha. Nimechoka kwa kuomba msaada, koo langu limekauka. Macho yangu yanafifia, nikimtafuta Mungu wangu. Wale wanaonichukia bila sababu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu; wengi ni adui kwangu bila sababu, wale wanaotafuta kuniangamiza. Ninalazimishwa kurudisha kitu ambacho sikuiba. Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu, wala hatia yangu haikufichika kwako. Ee Bwana, ewe BWANA Mwenye Nguvu Zote, wakutumainio wasiaibishwe kwa ajili yangu; wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli. Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako, aibu imefunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe. Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila, matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia. Ninapolia na kufunga, lazima nivumilie matusi. Ninapovaa nguo ya gunia, watu hunidharau. Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga, nimekuwa wimbo wa walevi. Lakini Ee BWANA, ninakuomba, kwa wakati ukupendezao; katika upendo wako mkuu, Ee Mungu, unijibu kwa wokovu wako wa hakika. Uniokoe katika matope, usiniache nizame; niokoe na hao wanichukiao, kutoka kwenye vilindi vya maji. Usiache mafuriko yanigharikishe au vilindi vinimeze, au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.