Zaburi 31:1-16
Zaburi 31:1-16 SRUV
Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Ngome thabiti ya kuniokoa. Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze na unichunge. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu. Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee BWANA, Mungu wa kweli. Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumainia BWANA. Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni, Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha mahali penye usalama. Ee BWANA, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu. Maana maisha yangu yamekwisha kwa huzuni, Na miaka yangu kwa maumivu. Nguvu zangu zimeniishia kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imepooza. Kwa sababu ya watesi wangu nimelaumiwa, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Wanaoniona njiani wananikimbia. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika. Maana nimesikia wengi wakinong'onezana; Hofu katika pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walipanga kunitoa uhai wangu. Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye kutoka kwa adui zangu na wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.