Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 31:1-16

Zaburi 31:1-16 NENO

Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe, kwa haki yako uniokoe. Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka; uwe kwangu mwamba wa kimbilio, ngome imara ya kuniokoa. Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu, uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako. Uniepushe na mtego niliotegewa, maana wewe ndiwe kimbilio langu. Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako, unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli. Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili; bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu. Nitafurahia na kushangilia upendo wako, kwa kuwa uliona mateso yangu na ulijua maumivu ya nafsi yangu. Hukunikabidhi kwa adui yangu bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi. Ee Mwenyezi Mungu unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida; macho yangu yanafifia kwa huzuni, nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko. Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi, naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali; nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso, na mifupa yangu inachakaa. Kwa sababu ya adui zangu wote, nimedharauliwa kabisa na majirani zangu, hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho, wale wanaoniona barabarani wananikimbia. Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa, nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika. Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi; vitisho viko pande zote; kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu, na kula njama kuniua. Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu; nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.” Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako, uniokoe mikononi mwa adui zangu na wale wanifuatiao. Mwangazie mtumishi wako uso wako, uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.