Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 31:1-14

Ezekieli 31:1-14 SRUV

Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako? Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akatuma vijito vyake kwa miti yote ya shambani. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya shambani, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. Ndege wote wa angani walifanya viota vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi. Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misonobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wowote uliofanana naye kwa uzuri. Nilimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu. Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake. Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika uvuli wake na kumwacha. Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani watakuwa juu ya matawi yake; ili mti wowote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.