Ezekieli 31:1-14
Ezekieli 31:1-14 NEN
Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake ya wajeuri: “ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa na wewe katika fahari. Angalia Ashuru, wakati fulani ilikuwa mwerezi huko Lebanoni, ukiwa na matawi mazuri ukitia msitu kivuli; ulikuwa mrefu sana, kilele chake kilipita majani ya miti yote. Maji mengi yaliustawisha, chemchemi zenye maji mengi ziliufanya urefuke; vijito vyake vilitiririka pale ulipoota pande zote na kupeleka mifereji yake kwenye miti yote ya shambani. Hivyo ukarefuka kupita miti yote ya shambani; vitawi vyake viliongezeka na matawi yake yakawa marefu, yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji. Ndege wote wa angani wakaweka viota kwenye vitawi vyake, wanyama wote wa shambani wakazaana chini ya matawi yake, mataifa makubwa yote yaliishi chini ya kivuli chake. Ulikuwa na fahari katika uzuri, ukiwa na matawi yaliyotanda, kwa kuwa mizizi yake ilikwenda chini mpaka kwenye maji mengi. Mierezi katika bustani ya Mungu haikuweza kushindana nao, wala misunobari haikuweza kulingana na vitawi vyake, wala miaramoni haikulinganishwa na matawi yake, wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu wa kulinganisha na uzuri wake. Niliufanya kuwa mzuri ukiwa na matawi mengi, ulionewa wivu na miti yote ya Edeni katika bustani ya Mungu. “ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake, niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye aushughulikie sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali, nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kwenye kivuli chake na kuuacha. Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake. Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale waendao shimoni.