Ezekieli 31:1-14
Ezekieli 31:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mwambie hivi Farao mfalme wa Misri na watu wake wote: Wewe wafanana na nini kwa ukuu wako? Wewe ni kama mwerezi wa Lebanoni wenye matawi mazuri na majani mengi na shina refu. Kilele chake kinafika hata mawinguni. Maji yaliustawisha, vilindi vya maji viliulisha. Mito ilibubujika mahali ulipoota, ikapeleka vijito kwenye miti yote ya msituni. “Kwa hiyo, ulirefuka sana kupita miti yote msituni; matawi yake yalizidi kuwa mengi na makubwa, kutokana na maji mengi mizizini mwake. Ndege wote waliweka viota matawini mwake, chini yake wanyama walizaliwa, mataifa yote makubwa yaliburudika kivulini mwake. Ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake, na kwa urefu wa matawi yake. Mizizi yake ilipenya chini mpaka penye maji mengi. Miongoni mwa mierezi ya bustanini mwa Mungu, hakuna mti uliolingana nao, wala misonobari haikulingana na matawi yake, mibambakofi haikuwa na matawi kama yake, hata mti wowote wa bustani ya Mungu haukulingana nao kwa uzuri. Mimi niliufanya kuwa mzuri kwa matawi yake mengi; ulionewa wivu na miti yote ya Edeni iliyokuwa katika bustani ya Mungu. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu wewe ulirefusha kimo chake na kukiinua kilele chake kati ya matawi makubwa, ukajivunia urefu wake, nitautia mikononi mwa mkuu kati ya mataifa. Yeye, atauadhibu. Nimeutupilia mbali kadiri ya uovu wake. Watu wa mataifa mengine katili kupindukia, wataukata na kuubwaga chini na kuuacha. Matawi yake yataanguka chini mlimani na kila mahali mabondeni; yatavunjika na kutapakaa chini katika magenge yote. Watu wote wataondoka kivulini mwake na kuuacha. Ndege wote watatua juu ya mabaki yake na wanyama wote wa porini watakanyaga matawi yake. Hayo yameupata ili mti wowote ulio mahali penye maji usiweze kurefuka tena kiasi hicho wala kukifikisha kilele chake mawinguni. Mti wowote unaonyweshwa maji usiweze tena kufikia urefu huo. Kwa maana kila kitu mwisho wake ni kifo; hali kadhalika na watu. Wote watashiriki hali yao washukao shimoni kwa wafu.
Ezekieli 31:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako? Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akatuma vijito vyake kwa miti yote ya shambani. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya shambani, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. Ndege wote wa angani walifanya viota vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi. Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misonobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wowote uliofanana naye kwa uzuri. Nilimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu. Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake. Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika uvuli wake na kumwacha. Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani watakuwa juu ya matawi yake; ili mti wowote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.
Ezekieli 31:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako? Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi. Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa uzuri. Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu. Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake. Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika uvuli wake na kumwacha. Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani watakuwa juu ya matawi yake; kusudi mti wo wote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.
Ezekieli 31:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake ya wajeuri: “ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa na wewe katika fahari. Angalia Ashuru, wakati fulani ilikuwa mwerezi huko Lebanoni, ukiwa na matawi mazuri ukitia msitu kivuli; ulikuwa mrefu sana, kilele chake kilipita majani ya miti yote. Maji mengi yaliustawisha, chemchemi zenye maji mengi ziliufanya urefuke; vijito vyake vilitiririka pale ulipoota pande zote na kupeleka mifereji yake kwenye miti yote ya shambani. Hivyo ukarefuka kupita miti yote ya shambani; vitawi vyake viliongezeka na matawi yake yakawa marefu, yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji. Ndege wote wa angani wakaweka viota kwenye vitawi vyake, wanyama wote wa shambani wakazaana chini ya matawi yake, mataifa makubwa yote yaliishi chini ya kivuli chake. Ulikuwa na fahari katika uzuri, ukiwa na matawi yaliyotanda, kwa kuwa mizizi yake ilikwenda chini mpaka kwenye maji mengi. Mierezi katika bustani ya Mungu haikuweza kushindana nao, wala misunobari haikuweza kulingana na vitawi vyake, wala miaramoni haikulinganishwa na matawi yake, wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu wa kulinganisha na uzuri wake. Niliufanya kuwa mzuri ukiwa na matawi mengi, ulionewa wivu na miti yote ya Edeni katika bustani ya Mungu. “ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake, niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye aushughulikie sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali, nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kwenye kivuli chake na kuuacha. Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake. Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale waendao shimoni.