Ezekieli 31:1-14
Ezekieli 31:1-14 BHN
Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mwambie hivi Farao mfalme wa Misri na watu wake wote: Wewe wafanana na nini kwa ukuu wako? Wewe ni kama mwerezi wa Lebanoni wenye matawi mazuri na majani mengi na shina refu. Kilele chake kinafika hata mawinguni. Maji yaliustawisha, vilindi vya maji viliulisha. Mito ilibubujika mahali ulipoota, ikapeleka vijito kwenye miti yote ya msituni. “Kwa hiyo, ulirefuka sana kupita miti yote msituni; matawi yake yalizidi kuwa mengi na makubwa, kutokana na maji mengi mizizini mwake. Ndege wote waliweka viota matawini mwake, chini yake wanyama walizaliwa, mataifa yote makubwa yaliburudika kivulini mwake. Ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake, na kwa urefu wa matawi yake. Mizizi yake ilipenya chini mpaka penye maji mengi. Miongoni mwa mierezi ya bustanini mwa Mungu, hakuna mti uliolingana nao, wala misonobari haikulingana na matawi yake, mibambakofi haikuwa na matawi kama yake, hata mti wowote wa bustani ya Mungu haukulingana nao kwa uzuri. Mimi niliufanya kuwa mzuri kwa matawi yake mengi; ulionewa wivu na miti yote ya Edeni iliyokuwa katika bustani ya Mungu. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu wewe ulirefusha kimo chake na kukiinua kilele chake kati ya matawi makubwa, ukajivunia urefu wake, nitautia mikononi mwa mkuu kati ya mataifa. Yeye, atauadhibu. Nimeutupilia mbali kadiri ya uovu wake. Watu wa mataifa mengine katili kupindukia, wataukata na kuubwaga chini na kuuacha. Matawi yake yataanguka chini mlimani na kila mahali mabondeni; yatavunjika na kutapakaa chini katika magenge yote. Watu wote wataondoka kivulini mwake na kuuacha. Ndege wote watatua juu ya mabaki yake na wanyama wote wa porini watakanyaga matawi yake. Hayo yameupata ili mti wowote ulio mahali penye maji usiweze kurefuka tena kiasi hicho wala kukifikisha kilele chake mawinguni. Mti wowote unaonyweshwa maji usiweze tena kufikia urefu huo. Kwa maana kila kitu mwisho wake ni kifo; hali kadhalika na watu. Wote watashiriki hali yao washukao shimoni kwa wafu.