Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 31

31
Mwerezi mrefu
1Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, 2Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako? 3#Nah 3:18; Sef 2:13 Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. 4Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akatuma vijito vyake kwa miti yote ya shambani. 5#Zab 37:35,36; Dan 4:11; Isa 10:7-11,13 Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya shambani, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. 6#Eze 17:23; Dan 4:12 Ndege wote wa angani walifanya viota vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. 7Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi. 8#Mwa 2:9 Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misonobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wowote uliofanana naye kwa uzuri. 9#Kut 9:16; Zab 75:6; Dan 4:22-24 Nilimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu.
10 # 2 Nya 25:19; Ayu 40:11,12; Mit 16:18; Isa 14:13-15; Eze 28:17; Dan 5:20; Yak 4:6 Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake; 11mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake. 12#Eze 28:7; 32:5 Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika uvuli wake na kumwacha. 13#Isa 18:6 Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani watakuwa juu ya matawi yake; 14#Zab 82:7; Eze 32:18 ili mti wowote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.
15Bwana MUNGU asema hivi, Katika siku ile alipoteremka mpaka kuzimu niliamuru matanga, nilikifunika kilindi kwa ajili yake, nikiizuia mito yake, nayo maji makuu yalizuiwa; niliamuru Lebanoni kumwombolezea, na miti yote ya shambani ilizimia kwa ajili yake. 16#Eze 26:15; 32:31; Isa 14:8,15 Niliwatetemesha mataifa kwa mshindo wa kuanguka kwake, hapo nilipomtupa chini mpaka kuzimu, pamoja nao washukao shimoni; na miti yote ya Adeni, miti iliyo miteule na iliyo mizuri ya Lebanoni, yote inywayo maji, ilifarijika pande za chini za nchi. 17#Omb 4:20 Hao nao waliteremka kuzimuni pamoja naye kwa watu waliouawa kwa upanga; naam, wale waliowasaidia,#31:17 Katika Kiebrania ni ‘mkono wake’. waliokaa chini ya uvuli wake kati ya mataifa.
18 # Eze 32:19; 28:10 Umefanana na nani, hivi katika utukufu na ukuu, kati ya miti ya Adeni? Lakini utashushwa pamoja na miti ya Adeni, hata pande za chini za nchi; utalala kati ya hao wasiotahiriwa; pamoja na hao waliouawa kwa upanga. Huyu ndiye Farao, na jamii yote ya watu wake, asema Bwana MUNGU.

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 31: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha