Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 22:38-51

2 Samweli 22:38-51 SRUV

Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita; Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea; Mara tu waliposikia habari zangu, Walinitii. Wageni nao waliishiwa nguvu, Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anilipiziaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake; Amfanyia fadhili masihi wake, Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.