Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 22:38-51

2 Samueli 22:38-51 BHN

Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza, sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa. Niliwaangamiza, nikawaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha adui chini yangu. Uliwafanya adui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa, walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani. “Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, umenifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea, mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wangu! Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi na kuyatiisha mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka adui zangu. Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu na kunisalimisha mbali na watu wakatili. “Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”