2 Samueli 22:38-51
2 Samueli 22:38-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza, sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa. Niliwaangamiza, nikawaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha adui chini yangu. Uliwafanya adui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa, walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani. “Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, umenifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea, mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wangu! Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi na kuyatiisha mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka adui zangu. Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu na kunisalimisha mbali na watu wakatili. “Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”
2 Samueli 22:38-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita; Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea; Mara tu waliposikia habari zangu, Walinitii. Wageni nao waliishiwa nguvu, Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anilipiziaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake; Amfanyia fadhili masihi wake, Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.
2 Samueli 22:38-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenifunga mshipi wa nguvu kwa vita; Umenitiishia chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hakuna wa kuokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni watanijia wakinyenyekea; Kwa kusikia tu habari zangu, Mara watanitii. Wageni nao watatepetea, Watatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anipatiaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kunileta nje nitoke kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Waniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu; Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake, hata milele.
2 Samueli 22:38-51 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa. Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani. “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia, nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu, aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako. “Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”