2 Samweli 22:38-51
2 Samweli 22:38-51 NENO
“Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa. Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani. “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia, nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu, aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako. “Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”