2 Samweli 22
22
Wimbo wa Daudi wa ushindi
(Zaburi 18)
1Daudi alimwimbia Mwenyezi Mungu maneno ya wimbo huu Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. 2Akasema:
“Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
3Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia,
ngao yangu na pembe#22:3 pembe inawakilisha nguvu ya wokovu wangu.
Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu,
huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
4“Ninamwita Mwenyezi Mungu, anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5Mawimbi ya mauti yalinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
6Kamba za Kuzimu#22:6 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho. zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
7“Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu,
nilimlilia Mungu wangu.
Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika masikioni mwake.
8Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya mbingu ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu
alikuwa amekasirika.
9Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yaliyowaka
yakatoka ndani yake.
10Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
12Alifanya giza hema lake la kujifunika:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
13Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mwanga wa radi ukatoka.
14Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15Aliipiga mishale na kutawanya adui,
akawafukuza kwa umeme mkubwa wa radi.
16Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwake Mwenyezi Mungu,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.
17“Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
18Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
19Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
20Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21“Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
22Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
24Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
25Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu,
sawasawa na usafi wangu machoni pake.
26“Kwa yeye aliye mwaminifu unajionesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionesha kutokuwa na hatia,
27kwa aliye mtakatifu unajionesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka unajionesha kuwa mkaidi.
28Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
29Wewe ni taa yangu, Ee Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
30Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
31“Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;
neno la Mwenyezi Mungu halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
32Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Mwenyezi Mungu?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
33Mungu ndiye anivikaye nguvu,
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
36Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu;
msaada wako umeniinua niwe mkuu.
37Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
38“Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta,
sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
39Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
41Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
42Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
43Niliwaponda kama mavumbi ya nchi;
niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.
44“Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;
umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.
Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45nao wageni huja wakininyenyekea,
mara wanisikiapo, hunitii.
46Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47“Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu!
48Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
ayawekaye mataifa chini yangu,
49aniwekaye huru toka kwa adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50Kwa hiyo nitakusifu, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51“Humpa mfalme wake ushindi mkuu;
huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.”
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 22: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.