Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 15:1-12

2 Samweli 15:1-12 SRUV

Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu yeyote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumishi wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli. Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza. Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au kesi aje kwangu, nimpatie haki yake! Tena ikawa hapo alipokaribia mtu yeyote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli. Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme, Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea BWANA huko Hebroni. Maana mimi mtumishi wako niliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama BWANA akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia BWANA. Naye mfalme akamwambia, Nenda kwa amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni. Lakini Absalomu akatuma wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anatawala huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lolote. Absalomu alipokuwa akitoa dhabihu alituma Ahithofeli Mgiloni, Mshauri wake Daudi, aitwe kutoka mji wake, yaani, Gilo. Njama zao zikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu walizidi kuongezeka.