2 Sam 15:1-12
2 Sam 15:1-12 SUV
Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli. Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza. Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake! Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli. Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea BWANA huko Hebroni. Maana mimi mtumishi wako naliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama BWANA akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia BWANA. Naye mfalme akamwambia, Enenda na amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni. Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.