2 Samueli 15:1-12
2 Samueli 15:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya tukio hilo, Absalomu alijipatia gari, farasi na watu hamsini wa kumtangulia. Absalomu alizoea kuamka asubuhi na mapema na kwenda kusimama kwenye njia inayoelekea kwenye lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na madai ambayo alitaka kuyapeleka kwa mfalme ili kupata uamuzi wake, Absalomu humwita mtu huyo kando na kumwuliza, “Unatoka mji gani?” Kama mtu huyo akisema ametoka mji fulani wa kabila la Israeli, Absalomu humwambia, “Madai yako ni ya haki kabisa. Lakini hakuna mtu yeyote aliyeteuliwa na mfalme kukusikiliza.” Tena, Absalomu humwambia, “Laiti mimi ningekuwa mwamuzi wa Israeli! Kila mtu mwenye madai au shauri angekuja kwangu, nami ningempa haki yake!” Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu. Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli. Baada ya miaka minne, Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu; maana, mimi mtumishi wako, nilipoishi kule Geshuri katika Aramu, nilimwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri nikisema kuwa kama Mwenyezi-Mungu atanirudisha mjini Yerusalemu basi, nitamwabudu yeye.” Mfalme akamwambia, “Basi, nenda kwa amani.” Absalomu akaondoka kwenda Hebroni. Lakini Absalomu alituma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, wakasema, “Mara moja mtakaposikia mlio wa tarumbeta, semeni, ‘Absalomu ni mfalme katika Hebroni!’” Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.
2 Samueli 15:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu yeyote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumishi wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli. Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza. Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au kesi aje kwangu, nimpatie haki yake! Tena ikawa hapo alipokaribia mtu yeyote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli. Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme, Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea BWANA huko Hebroni. Maana mimi mtumishi wako niliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama BWANA akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia BWANA. Naye mfalme akamwambia, Nenda kwa amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni. Lakini Absalomu akatuma wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anatawala huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lolote. Absalomu alipokuwa akitoa dhabihu alituma Ahithofeli Mgiloni, Mshauri wake Daudi, aitwe kutoka mji wake, yaani, Gilo. Njama zao zikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu walizidi kuongezeka.
2 Samueli 15:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli. Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza. Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake! Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli. Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea BWANA huko Hebroni. Maana mimi mtumishi wako naliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama BWANA akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia BWANA. Naye mfalme akamwambia, Enenda na amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni. Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.
2 Samueli 15:1-12 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya muda, Absalomu akajipatia magari ya vita na farasi pamoja na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Akawa anaamka asubuhi na mapema na kusimama kando ya barabara inayoelekea kwenye lango la mji. Wakati wowote alipokuja mtu yeyote mwenye mashtaka yanayohitaji kuletwa mbele ya mfalme kwa maamuzi, Absalomu naye angemwita na kumuuliza, “Wewe unatoka mji upi?” Naye angejibu, “Mtumishi wako anatoka katika mojawapo ya makabila ya Israeli.” Kisha Absalomu angemwambia, “Tazama, malalamiko yako ni ya haki na sawasawa, lakini hakuna mwakilishi wa mfalme wa kukusikiliza.” Absalomu aliongeza, “Laiti tu ningeteuliwa kuwa mwamuzi katika nchi. Ndipo kila mmoja mwenye mashtaka au shauri angekuja kwangu nami ningeona kwamba anapata haki.” Pia, wakati mtu yeyote alipomkaribia ili kusujudu mbele yake, Absalomu alinyoosha mkono wake, na kumkumbatia na kumbusu. Absalomu akaendelea na tabia hii mbele ya Waisraeli wote waliomjia mfalme kumwomba awape haki; kwa hiyo Absalomu akavutia mioyo ya watu wa Israeli. Hapo mwisho wa mwaka wa nne, Absalomu akamwambia mfalme, “Naomba unipe ruhusa niende Hebroni nikatimize nadhiri niliyomwekea Mwenyezi Mungu. Mtumishi wako alipokuwa huko Geshuri katika nchi ya Aramu, niliweka nadhiri hii: ‘Ikiwa Mwenyezi Mungu atanirudisha Yerusalemu, nitamwabudu Mwenyezi Mungu huko Hebroni.’ ” Mfalme akamwambia, “Nenda kwa amani.” Hivyo akaenda Hebroni. Kisha Absalomu akatuma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, kusema, “Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta basi semeni, ‘Absalomu ni mfalme huko Hebroni.’ ” Watu mia mbili kutoka Yerusalemu walikuwa wamefuatana na Absalomu. Walikuwa wamealikwa kama wageni nao walienda kwa nia njema, pasipo kujua lolote. Absalomu alipokuwa anatoa dhabihu, pia akatuma aitwe Ahithofeli Mgiloni, mshauri wa Daudi, aje kutoka Gilo, ambao ndio mji wake wa nyumbani. Kwa hiyo mpango wa hila ukapata nguvu, na idadi ya waliofuatana na Absalomu ikaongezeka.