Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 15:1-12

2 Samweli 15:1-12 NENO

Baada ya muda, Absalomu akajipatia magari ya vita na farasi pamoja na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Akawa anaamka asubuhi na mapema na kusimama kando ya barabara inayoelekea kwenye lango la mji. Wakati wowote alipokuja mtu yeyote mwenye mashtaka yanayohitaji kuletwa mbele ya mfalme kwa maamuzi, Absalomu naye angemwita na kumuuliza, “Wewe unatoka mji upi?” Naye angejibu, “Mtumishi wako anatoka katika mojawapo ya makabila ya Israeli.” Kisha Absalomu angemwambia, “Tazama, malalamiko yako ni ya haki na sawasawa, lakini hakuna mwakilishi wa mfalme wa kukusikiliza.” Absalomu aliongeza, “Laiti tu ningeteuliwa kuwa mwamuzi katika nchi. Ndipo kila mmoja mwenye mashtaka au shauri angekuja kwangu nami ningeona kwamba anapata haki.” Pia, wakati mtu yeyote alipomkaribia ili kusujudu mbele yake, Absalomu alinyoosha mkono wake, na kumkumbatia na kumbusu. Absalomu akaendelea na tabia hii mbele ya Waisraeli wote waliomjia mfalme kumwomba awape haki; kwa hiyo Absalomu akavutia mioyo ya watu wa Israeli. Hapo mwisho wa mwaka wa nne, Absalomu akamwambia mfalme, “Naomba unipe ruhusa niende Hebroni nikatimize nadhiri niliyomwekea Mwenyezi Mungu. Mtumishi wako alipokuwa huko Geshuri katika nchi ya Aramu, niliweka nadhiri hii: ‘Ikiwa Mwenyezi Mungu atanirudisha Yerusalemu, nitamwabudu Mwenyezi Mungu huko Hebroni.’ ” Mfalme akamwambia, “Nenda kwa amani.” Hivyo akaenda Hebroni. Kisha Absalomu akatuma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, kusema, “Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta basi semeni, ‘Absalomu ni mfalme huko Hebroni.’ ” Watu mia mbili kutoka Yerusalemu walikuwa wamefuatana na Absalomu. Walikuwa wamealikwa kama wageni nao walienda kwa nia njema, pasipo kujua lolote. Absalomu alipokuwa anatoa dhabihu, pia akatuma aitwe Ahithofeli Mgiloni, mshauri wa Daudi, aje kutoka Gilo, ambao ndio mji wake wa nyumbani. Kwa hiyo mpango wa hila ukapata nguvu, na idadi ya waliofuatana na Absalomu ikaongezeka.