Ufunuo 2
2
Kwa kundi la waumini lililoko Efeso
1“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Efeso, andika:
Haya ndio maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.
2Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewajaribu wale wanaojifanya mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka. 4Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. 5Kumbuka basi ni wapi ulikoanguka! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. 6Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.
7Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda ya uzima, ambao uko katika paradiso#2:7 Paradiso maana yake bustani nzuri ya Mungu.
Kwa kundi la waumini lililoko Smirna
8“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Smirna, andika:
Haya ndio maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.
9Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi#2:9 Nyumba ya ibada na mafunzo. la Shetani. 10Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji la uzima.
11Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye hatadhuriwa kamwe na mauti ya pili.
Kwa kundi la waumini lililoko Pergamo
12“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Pergamo, andika:
Haya ndio maneno yake yeye aliye na upanga mkali wenye makali kuwili.
13Ninajua unakoishi: kule Shetani ana kiti chake cha utawala. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu, hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji wenu mkuu, anakoishi Shetani. 14Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na kufanya uasherati. 15Vivyo hivyo unao wale wanaoyashikilia mafundisho ya Wanikolai. 16Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.
17Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.
Kwa kundi la waumini lililoko Thiatira
18“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Thiatira, andika:
Haya ndio maneno ya Mwana wa Mungu#2:18 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., ambaye macho yake ni kama mwali wa moto, na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa.
19Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako, na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza. 20Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. 21Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. 22Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. 23Nami nitawaua watoto wake. Nayo makundi yote ya waumini yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. 24Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu): 25Lakini shikeni sana mlicho nacho, hadi nitakapokuja. 26Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu hadi mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa: 27‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’#2:27 Zaburi 2:9: kama mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. 28Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.
29Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
Iliyochaguliwa sasa
Ufunuo 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.