Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 1

1
Utangulizi
1Ufunuo wa Isa Al-Masihi aliopewa na Mungu ili awaoneshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake, 2ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichokiona, yaani neno la Mungu na ushuhuda wa Isa Al-Masihi. 3Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.
Salamu kwa makundi saba ya waumini
4Yohana.
Kwa makundi saba ya waumini yaliyo jimbo la Asia.
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyeko, aliyekuwako, na atakayekuja, na kutoka kwa wale roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, 5na kutoka kwa Isa Al-Masihi, aliye shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, mtawala wa wafalme wa dunia.
Kwake yeye anayetupenda na aliyetuweka huru kutoka dhambi zetu kwa damu yake, 6na akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, ili tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba#1:6 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yake. Utukufu na uwezo ni vyake milele na milele! Amen.
7“Tazama! Anakuja na mawingu,”#1:7 Danieli 7:13
na “kila jicho litamwona,
hata wale waliomchoma”#1:7 Zekaria 12:10;
na makabila yote duniani
“yataomboleza kwa sababu yake.”
Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.
8“Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mwenyezi Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”
Maono ya Al-Masihi
9Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Isa na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Isa. 10Katika Siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho wa Mungu na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu 11ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makundi saba ya waumini: kwa Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, 13na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu#1:13 Danieli 7:13, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake. 14Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. 15Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayong’aa katika tanuru la moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mngurumo wa maji mengi. 16Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua liking’aa kwa nguvu zake zote.
17Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na Kuzimu#1:18 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu..
19“Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya. 20Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makundi saba ya waumini, navyo vile vinara saba ni hayo makundi saba.

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia