Ufunuo 3
3
Kwa kundi la waumini lililoko Sardi
1“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Sardi, andika:
Haya ndio maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu#3:1 Roho saba za Mwenyezi Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake. na zile nyota saba.
Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa. 2Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. 3Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia; yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako. 4Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. 5Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba#3:5 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu na mbele za malaika wake.
6Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
Kwa kundi la waumini lililoko Filadelfia
7“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Filadelfia, andika:
Haya ndio maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.
8Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu. 9Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, nitawafanya waje wapige magoti miguuni pako, na wakiri kwamba nimekupenda. 10Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wanaoishi duniani. 11Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akalichukua taji lako. 12Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji mkubwa wa Mungu wangu, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya.
13Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.
Kwa kundi la waumini lililoko Laodikia
14“Kwa malaika wa kundi la waumini lililoko Laodikia, andika:
Haya ndio maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.
15Nayajua matendo yako, kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa moto au baridi. 16Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona. 19Wale ninaowapenda, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami. 21Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.
22Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho wa Mungu ayaambia makundi ya waumini.”
Iliyochaguliwa sasa
Ufunuo 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.