Ufunuo 12
12
Mwanamke na joka
1Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na taji lenye nyota kumi na mbili lilikuwa kichwani mwake. 2Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi, na taji saba katika vichwa vyake. 4Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo ya utawala ya chuma#12:5 Zaburi 2:9. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. 6Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini.
Malaika Mikaeli amshinda joka
7Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika wake likapigana nao. 8Lakini joka na malaika wake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika wake.
Ushindi mbinguni watangazwa
10Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:
“Sasa wokovu na uweza na ufalme wa Mungu wetu Mwenyezi umekuja,
na mamlaka ya Al-Masihi wake.
Kwa kuwa ametupwa chini
mshtaki wa ndugu zetu,
anayewashtaki mbele za Mungu
usiku na mchana.
11Nao wakamshinda
kwa damu ya Mwana-Kondoo
na kwa neno la ushuhuda wao.
Wala wao hawakuyapenda maisha yao sana,
hata wakawa tayari kufa.
12Kwa hiyo furahini, ninyi mbingu
na wote wanaoishi humo!
Lakini ole wenu nchi na bahari,
kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu,
akiwa amejaa ghadhabu,
kwa sababu anajua ya kuwa
muda wake ni mfupi!”
13Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto wa kiume. 14Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka hadi mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, ya wakati ambako lile joka haliwezi kufika. 15Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke, achukuliwe na mafuriko. 16Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao lile joka lilikuwa limeutoa kinywani mwake. 17Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na wazawa waliosalia wa huyo mwanamke, yaani wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Isa Al-Masihi.
Iliyochaguliwa sasa
Ufunuo 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.