Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 11

11
Mashahidi wawili
1Ndipo nikapewa mwanzi uliokuwa kama ufito wa kupimia, nikaambiwa, “Nenda ukapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo. 2Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu; uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu wa Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na mbili. 3Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini, wakiwa wamevaa gunia.” 4Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wa dunia yote#11:4 Zekaria 4:3, 11, 14. 5Kama mtu yeyote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu yeyote atakayetaka kuwadhuru. 6Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo.
7Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua. 8Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa#11:8 yaani Yerusalemu, ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo pia Isa Bwana wao alisulubiwa. 9Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu zizikwe. 10Watu wanaoishi duniani watazitazama maiti za hao manabii wawili kwa furaha, na kushangilia kwa kupeana zawadi, kwa sababu hao manabii waliwatesa watu wanaoishi duniani.
11Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. 12Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama.
13Saa hiyo hiyo, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
14Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.
Tarumbeta ya saba
15Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema:
“Ufalme wa ulimwengu umekuwa
ufalme wa Bwana wetu na wa Al-Masihi wake,
naye atatawala milele na milele.”
16Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya utawala, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, 17wakisema:
“Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi,
uliyeko na uliyekuwako,
kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu
na ukaanza kutawala.
18Mataifa walikasirika;
nao wakati wa ghadhabu yako umewadia.
Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa,
na kuwapa thawabu watumishi wako manabii,
na watakatifu wako pamoja na wale wote
wanaoliheshimu Jina lako,
wakubwa kwa wadogo:
na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”
19Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake likaonekana humo. Kukatokea miali ya radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la ardhi na mvua kubwa ya mawe.

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 11: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia