Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 13

13
1Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.
Mnyama kutoka baharini
Nami nikamwona mnyama akitoka ndani ya bahari. Mnyama huyo alikuwa na pembe kumi na vichwa saba, akiwa na taji kumi kwenye hizo pembe zake, na juu ya kila kichwa kulikuwa na jina la kukufuru. 2Mnyama yule niliyemwona alifanana na chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ya dubu na kichwa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu zake, kiti chake cha utawala na mamlaka makubwa. 3Mojawapo ya vichwa vya huyo mnyama kilikuwa kama kilichokwisha kupata jeraha la mauti, lakini jeraha hilo la mauti likapona. Ulimwengu wote ukashangaa ukamfuata huyo mnyama. 4Watu wakaliabudu lile joka kwa sababu lilikuwa limempa huyo mnyama mamlaka yake, pia wakamwabudu huyo mnyama na kuuliza, “Ni nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana vita naye?”
5Huyo mnyama akapewa mdomo wa kusema maneno ya kiburi na kukufuru, na uwezo wa kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na mbili. 6Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wanaokaa mbinguni. 7Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa. 8Nao watu wote wanaoishi duniani watamwabudu huyo mnyama: wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
9Yeye aliye na sikio na asikie.
10“Ikiwa mtu ni wa kuchukuliwa mateka,
atachukuliwa mateka.
Ikiwa mtu ni wa kuuawa kwa upanga,
atauawa kwa upanga.”#13:10 Yeremia 15:2
Hapa ndipo penye wito wa subira na imani ya watakatifu.
Mnyama kutoka ardhini
11Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka. 12Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akaifanya dunia na wote walioishi duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. 13Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. 14Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya watu walioishi duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi. 15Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa. 16Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye paji la uso wake, 17ili mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake.
18Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni mia sita sitini na sita (666).

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia