Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 14

14
Mwana-Kondoo na wale 144,000
1Kisha nikatazama, na hapo mbele yangu Mwana-Kondoo alikuwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale elfu mia moja na arobaini na nne wenye jina la Mwana-Kondoo na jina la Baba#14:1 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yake limeandikwa kwenye paji za nyuso zao. 2Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. 3Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi, na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai, na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao elfu mia moja na arobaini na nne waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. 4Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. 5Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.
Malaika watatu
6Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale wanaoishi duniani: kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. 7Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”
8Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu#14:8 Isaya 21:9, mji ule ulioyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”
9Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye paji la uso wake au kwenye mkono wake, 10yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” 12Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Isa.
13Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Isa Bwana tangu sasa.”
“Naam,” asema Roho wa Mungu, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”
Kuvuna mavuno ya dunia
14Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa kama Mwana wa Adamu#14:14 Danieli 7:13, akiwa na taji la dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. 15Kisha malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.” 16Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.
17Malaika mwingine akatoka katika Hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. 18Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” 19Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi#14:20 ni kama mita moja na nusu, kwa umbali wa maili mia moja na themanini#14:20 yamkini kilomita mia tatu na ishirini.

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia