Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 94

94
Zaburi 94
Mwenyezi Mungu, Mlipiza kisasi kwa ajili ya wenye haki
1Ee Mwenyezi Mungu, ulipizaye kisasi,
Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
2Ee Mhukumu wa dunia, inuka,
uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
3Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini waovu,
hadi lini waovu watashangilia?
4Wanamimina maneno ya kiburi,
watenda maovu wote wamejaa majivuno.
5Ee Mwenyezi Mungu, wanawaponda watu wako;
wanawatesa walio urithi wako.
6Wanamchinja mjane na mgeni,
na kuwaua yatima.
7Nao husema, “Mwenyezi Mungu haoni,
Mungu wa Yakobo hafahamu.”
8Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu;
enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
9Je, aliyeweka sikio asisikie?
Aliyeumba jicho asione?
10Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?
Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11Mwenyezi Mungu anajua mawazo ya mwanadamu;
anajua kwamba ni ubatili.
12Ee Mwenyezi Mungu, heri mtu anayeadhibishwa na wewe,
mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
13unampa utulivu siku za shida,
hadi shimo litakapokuwa limechimbwa
kwa ajili ya mwovu.
14Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatawakataa watu wake,
hatauacha urithi wake.
15Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,
wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
16Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?
Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
17Kama Mwenyezi Mungu hangenisaidia upesi,
ningeishi katika kimya cha kifo.
18Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”
Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako ulinishikilia.
19Wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,
faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
20Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,
ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
21Huungana kuwashambulia wenye haki,
kuwahukumu kufa wasio na hatia.
22Lakini Mwenyezi Mungu amekuwa ngome yangu,
na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
23Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao
na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;
Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, atawaangamiza.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 94: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia