Mithali 30:7-17
Mithali 30:7-17 NEN
“Ninakuomba vitu viwili, Ee BWANA; usininyime kabla sijafa: Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo; usinipe umaskini wala utajiri, bali unipe chakula cha kunitosha kila siku. Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana na kusema, ‘BWANA ni nani?’ Au nisije nikawa maskini nikaiba, nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu. “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake, asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo. “Wako watu wale ambao huwalaani baba zao na wala hawawabariki mama zao; wale ambao ni safi machoni pao wenyewe kumbe hawakuoshwa uchafu wao; wale ambao daima macho yao ni ya kiburi, ambao kutazama kwao ni kwa dharau; wale ambao meno yao ni panga na ambao mataya yao yamewekwa visu kuwaangamiza maskini katika nchi, na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu. “Mruba anao binti wawili waliao, ‘Nipe! Nipe!’ “Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe, naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’: Ni kaburi, tumbo lisilozaa, nchi isiyoshiba maji kamwe, na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’ “Jicho lile limdhihakilo baba, lile linalodharau kumtii mama, litangʼolewa na kunguru wa bondeni, litaliwa na tai.