Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 6

6
Mnadhiri
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama Mnadhiri, 3ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu. 4Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.
5“ ‘Kwa muda wote wa nadhiri yake ya kujitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wembe hautapita kichwani mwake. Ni lazima awe mtakatifu hadi kipindi cha kujitenga kwake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kiishe; ni lazima aache nywele za kichwa chake zirefuke. 6Kwa kipindi chochote cha kujitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mnadhiri hatakaribia maiti. 7Hata kama baba yake mwenyewe au mama au kaka au dada akifa, hatajinajisi mwenyewe kwa ajili yao, kwa sababu ishara ya kujiweka wakfu kwake kwa Mungu ipo katika kichwa chake. 8Kwa kipindi chote cha kujitenga kwake, yeye ni wakfu kwa Mwenyezi Mungu.
9“ ‘Kama mtu yeyote akifa ghafula karibu na Mnadhiri, atakuwa ametiwa unajisi nywele zake alizoziweka wakfu, hivyo ni lazima anyoe nywele zake siku ya utakaso wake, yaani siku ya saba. 10Kisha siku ya nane ni lazima alete hua wawili au makinda wawili wa njiwa kwa kuhani katika mlango wa Hema la Kukutania. 11Kuhani atatoa mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Mnadhiri kwa sababu ametenda dhambi kwa kuwa mbele ya maiti. Siku hiyo hiyo atakiweka wakfu tena kichwa chake. 12Ni lazima ajitoe kabisa kwa Mwenyezi Mungu kwa kipindi cha kujitenga kwake, na ni lazima atoe mwana-kondoo wa kiume wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya hatia. Siku zilizopita hazitahesabiwa kwa sababu alijitia unajisi katika siku zake za kujitenga.
13“ ‘Basi hii ndiyo sheria kwa ajili ya Mnadhiri baada ya kipindi chake cha kujitenga kupita. Ataletwa kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 14Hapo atatoa sadaka zake kwa Mwenyezi Mungu: mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya amani, 15pamoja na sadaka zake za nafaka na za vinywaji, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, yaani maandazi yaliyotengenezwa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.
16“ ‘Kuhani atavileta vitu hivyo mbele za Mwenyezi Mungu na kufanya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa. 17Ataleta pia kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, na atatoa dhabihu kondoo dume kuwa sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka yake ya nafaka, na ya kinywaji.
18“ ‘Kisha kwenye ingilio la Hema la Kukutania, Mnadhiri ni lazima anyoe nywele zake ambazo alikuwa ameziweka wakfu. Atazichukua hizo nywele na kuziweka ndani ya moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka ya amani.
19“ ‘Baada ya Mnadhiri kunyoa hizo nywele zake za kujitenga kwake, kuhani atampa mikononi mwake bega la kondoo dume lililochemshwa, na pia andazi na mkate mwembamba kutoka kikapu, vyote vikiwa vimetengenezwa bila kuwekwa chachu. 20Kisha kuhani ataviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichoinuliwa, na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.
21“ ‘Hii ndiyo sheria ya Mnadhiri ambaye anaweka nadhiri kwa matoleo yake kwa Mwenyezi Mungu kufuatana na kujitenga kwake, zaidi ya chochote kile anachoweza kupata. Ni lazima atimize nadhiri aliyoiweka kufuatana na sheria ya Mnadhiri.’ ”
Baraka ya kikuhani
22Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 23“Mwambie Haruni na wanawe, ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni:
24“ ‘ “Mwenyezi Mungu akubariki
na kukulinda;
25Mwenyezi Mungu akuangazie nuru ya uso wake
na kukufadhili;
26Mwenyezi Mungu akugeuzie uso wake
na kukupa amani.” ’
27“Hivyo wataliweka Jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 6: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia