Hesabu 5
5
Utakaso wa kambi
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Waamuru Waisraeli kumtoa nje ya kambi mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi uambukizao#5:2 yaani ukoma, au anayetokwa na majimaji ya aina yoyote, au ambaye ni najisi kwa sababu ya maiti. 3Hii itakuwa ni kwa wote, yaani wanaume na wanawake; watoeni nje ya kambi ili wasije wakanajisi kambi yao, ambamo ninaishi miongoni mwao”. 4Waisraeli wakafanya hivyo; wakawatoa nje ya kambi. Wakafanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwelekeza Musa.
Malipo kwa ajili ya makosa
5Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 6“Waambie Waisraeli, ‘Mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu, mtu huyo ana hatia, 7na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea. 8Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye malipo yanaweza kufanywa kwa ajili ya kosa, malipo yatakuwa mali ya Mwenyezi Mungu, nayo ni lazima apewe kuhani, pamoja na kondoo dume ambaye anatumika kufanyia upatanisho kwa ajili yake. 9Matoleo yote matakatifu ya Waisraeli wanayoleta kwa kuhani yatakuwa yake. 10Kila kitu cha mtu kilichowekwa wakfu ni chake mwenyewe, lakini kile atoacho kwa kuhani kitakuwa cha kuhani.’ ”
Jaribio kwa ajili ya mke asiye mwaminifu
11Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 12“Nena na Waisraeli uwaambie: ‘Ikiwa mke wa mtu amepotoka na si mwaminifu kwa mumewe, 13kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine, tendo hili likafichika kwa mumewe na unajisi wake usigundulike (kwa kuwa hakuna ushahidi dhidi yake, naye hakukamatwa katika tendo hilo), 14nazo hisia za wivu zikamjia mumewe na kumshuku mkewe, naye mke yule ni najisi, au mumewe ana wivu na akamshuku ingawa si najisi, 15basi atampeleka mkewe kwa kuhani. Huyo mume itampasa apeleke pia sadaka ya unga wa shayiri kiasi cha sehemu ya kumi ya efa#5:15 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja. kwa niaba ya mkewe. Huyo mwanaume kamwe asimimine mafuta juu ya huo unga wala asiweke uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, sadaka ya ukumbusho ili kukumbushia uovu.
16“ ‘Kuhani atamleta huyo mwanamke na kumsimamisha mbele za Mwenyezi Mungu. 17Kisha kuhani atachukua sehemu ya maji matakatifu ndani ya gudulia la udongo na kuchanganya na baadhi ya vumbi kutoka sakafu ya Maskani. 18Baada ya kuhani kumsimamisha huyo mwanamke mbele za Mwenyezi Mungu, atazifungua nywele za huyo mwanamke na kuweka sadaka ya ukumbusho mikononi mwake, ile sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, huku kuhani mwenyewe akishikilia yale maji machungu yaletayo laana. 19Kisha kuhani atamwapiza huyo mwanamke, akimwambia, “Ikiwa hakuna mwanaume mwingine aliyekutana kimwili nawe, wala hujapotoka na kuwa najisi wakati ukiwa umeolewa na mumeo, maji haya machungu yaletayo laana na yasikudhuru. 20Lakini ikiwa umepotoka wakati ukiwa umeolewa na mume wako na umejinajisi mwenyewe kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine asiyekuwa mumeo”; 21hapa kuhani atamweka huyo mwanamke chini ya laana ya kiapo akisema: “Mwenyezi Mungu na awafanye watu wako wakulaani na kukukataa, wakati Mwenyezi Mungu atakapolifanya paja lako kupooza na tumbo lako kuvimba. 22Maji haya yaletayo laana na yaingie ndani ya mwili wako ili tumbo lako livimbe na paja lako lipooze.”
“ ‘Kisha mwanamke atasema, “Amen. Iwe hivyo.”
23“ ‘Kuhani ataandika laana hizi kwenye kitabu, kisha atazioshea laana hizo kwenye yale maji machungu. 24Kuhani atamnywesha yule mwanamke yale maji machungu yaletayo laana, nayo maji haya yatamwingia na kumsababishia maumivu makali. 25Kuhani atachukua sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu kutoka mikononi mwa huyo mwanamke, naye ataipunga mbele za Mwenyezi Mungu na kuileta madhabahuni. 26Kisha kuhani atachota sadaka ya nafaka mkono uliojaa kama sehemu ya kumbukumbu na kuiteketeza juu ya madhabahu, baada ya hayo, atamtaka huyo mwanamke anywe yale maji. 27Kama amejitia unajisi na kukosa uaminifu kwa mumewe, wakati anapotakiwa anywe maji yale yaletayo laana, yatamwingia na kusababisha maumivu makali; tumbo lake litavimba na paja lake litapooza, naye atakuwa amelaaniwa miongoni mwa watu wake. 28Hata hivyo, ikiwa huyo mwanamke hakujitia unajisi, naye ni safi, atasafishwa hatia na ataweza kuzaa watoto.
29“ ‘Basi, hii ndiyo sheria ya wivu mwanamke anapopotoka na kujitia unajisi akiwa ameolewa na mumewe, 30au hisia za wivu zinapomjia mwanaume kwa sababu ya kumshuku mkewe. Kuhani atamfanya huyo mwanamke kusimama mbele za Mwenyezi Mungu na atatumia sheria hii yote kwa huyo mwanamke. 31Mume atakuwa hana hatia ya kosa lolote, bali mwanamke atayachukua matokeo ya dhambi yake.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Hesabu 5: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.