Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 4

4
Wakohathi
1Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni, 2“Wahesabu Wakohathi walio sehemu ya Walawi kwa koo zao na jamaa zao. 3Wahesabu wanaume wote wenye umri wa miaka thelathini hadi hamsini wanaokuja kutumika katika kazi ya Hema la Kukutania.
4“Hii ndiyo kazi ya Wakohathi katika Hema la Kukutania: Watatunza vitu vilivyo vitakatifu sana. 5Kambi inapohamishwa, Haruni na wanawe wataingia ndani na kushusha lile pazia la kuzuilia na kufunika nalo Sanduku la Ushuhuda. 6Kisha watafunika juu yake na ngozi za pomboo#4:6 pengine ni mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili, na kutandaza juu yake kitambaa cha rangi ya buluu iliyokolea na kuingiza mipiko mahali pake.
7“Juu ya meza ya mikate ya Wonesho watatandaza kitambaa cha buluu na waweke sahani juu yake, masinia, bakuli na magudulia kwa ajili ya sadaka za kinywaji; mkate ule ambao upo hapa daima utabaki juu yake. 8Juu ya hivyo vitu watatandaza kitambaa chekundu na kufunika kwa ngozi za pomboo na kuweka mipiko yake mahali pake.
9“Watachukua kitambaa cha buluu na kufunika kinara cha taa kilicho kwa ajili ya nuru, pamoja na taa zake, mikasi yake, sinia zake, magudulia yake yote yaliyotumika kuwekea mafuta. 10Kisha watakisokotea pamoja na vifaa vyake vyote katika ngozi za pomboo na kukiweka kwenye jukwaa lake.
11“Juu ya madhabahu ya dhahabu watatandaza kitambaa cha buluu na kukifunika kwa ngozi za pomboo na kuweka mipiko yake mahali pake.
12“Watavichukua vyombo vyote vinavyotumika kuhudumia mahali patakatifu, watavisokotea kwenye kitambaa cha buluu na kufunika kwa ngozi za pomboo, na kuviweka juu ya miti ya kuchukulia.
13“Wataondoa majivu kutoka madhabahu ya shaba na kutandaza kitambaa cha zambarau juu yake. 14Kisha wataweka vyombo vyote juu yake vinavyotumika kwa kuhudumia madhabahuni pamoja na vyombo vya kutolea moto, nyuma, miiko na mabakuli ya kunyunyizia. Juu yake watatandaza ngozi za pomboo ya kufunika, na kuweka mipiko mahali pake.
15“Baada ya Haruni na wanawe kumaliza kazi ya kufunika samani takatifu na vyombo vyake vyote, watu watakapokuwa tayari kung’oa kambi, Wakohathi watakuja kufanya kazi ya kubeba. Lakini wasije wakagusa vitu vitakatifu la sivyo watakufa. Wakohathi ndio watakaobeba vile vitu vilivyomo katika Hema la Kukutania.
16“Eleazari mwana wa Haruni, kuhani, ndiye atakayesimamia mafuta kwa ajili ya taa, uvumba wenye harufu nzuri, sadaka za kila siku za nafaka na mafuta ya upako. Ndiye atakayekuwa msimamizi wa maskani yote ya Mungu na kila kitu kilicho ndani yake, pamoja na samani takatifu na vyombo vyake.”
17Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni, 18“Hakikisheni kwamba koo za kabila la Wakohathi hawatengwi kutoka Walawi. 19Ili wapate kuishi wala wasife wanapokaribia vitu vitakatifu sana, uwafanyie hivi: Haruni na wanawe wataenda mahali patakatifu na kumgawia kila mtu kazi yake, na kwamba ni nini atakachochukua. 20Lakini Wakohathi hawaruhusiwi kuingia ndani ili kuangalia vitu vitakatifu, hata kwa kitambo kidogo, la sivyo watakufa.”
Wagershoni
21Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 22“Wahesabu pia Wagershoni kwa jamaa zao na koo zao. 23Wahesabu wanaume wote wenye umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao huja kutumika katika Hema la Kukutania.
24“Hii ndiyo huduma ya koo za Wagershoni wakati wanapofanya kazi na kubeba mizigo. 25Watabeba mapazia ya maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, kifuniko chake na kifuniko cha nje cha ngozi za pomboo, mapazia ya maingilio ya Hema la Kukutania, 26mapazia ya ua unaozunguka Maskani na madhabahu, pazia la maingilio, kamba na vifaa vyote vinavyotumika katika huduma yake. Wagershoni watafanya yote yatakiwayo kufanyika na vitu hivi. 27Utumishi wao wote ukiwa ni kuchukua au wa kufanya kazi nyingine, utafanyika chini ya maelekezo ya Haruni na wanawe. Mtawapangia kama wajibu wao yote watakayoyafanya. 28Hii ndiyo huduma ya koo za Wagershoni katika Hema la Kukutania. Wajibu wao utakuwa chini ya maelekezo ya Ithamari mwana wa kuhani Haruni.
Wamerari
29“Wahesabu Wamerari kwa koo zao na jamaa zao. 30Wahesabu wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao watakuja kutumika katika Hema la Kukutania. 31Huu ndio wajibu wao wanapofanya huduma katika Hema la Kukutania: kubeba miimo ya Maskani, mataruma yake, nguzo na vitako, 32nguzo za ua unaozunguka pamoja na vitako vyake, vigingi vya hema, kamba, vifaa vyake vyote na kila kitu kinachohusiana na matumizi yake. Kila mtu mpangie vitu maalum vya kubeba. 33Huu ndio utumishi wa koo za Merari kama watakavyofanya kazi katika Hema la Kukutania, chini ya maelekezo ya Ithamari mwana wa kuhani, Haruni.”
Kuhesabiwa kwa koo za Walawi
34Musa, Haruni na viongozi wa jumuiya wakawahesabu Wakohathi kwa koo zao na jamaa zao.
35Wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania, 36waliohesabiwa kwa koo zao, walikuwa elfu mbili na mia saba hamsini (2,750). 37Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wote wale wa koo za Wakohathi ambao walitumika katika Hema la Kukutania. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatana na amri ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
38Wagershoni walihesabiwa kwa koo zao na jamaa zao.
39Watu wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania, 40waliohesabiwa kwa koo zao na jamaa zao, walikuwa elfu mbili na mia sita na thelathini (2,630). 41Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wale wa koo za Gershoni ambao walitumika katika Hema la Kukutania. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatana na amri ya Mwenyezi Mungu.
42Wamerari walihesabiwa kwa koo zao na jamaa zao.
43Wanaume wote kuanzia umri wa miaka thelathini hadi miaka hamsini ambao walikuja kutumika katika Hema la Kukutania, 44waliohesabiwa kwa koo zao, walikuwa elfu tatu na mia mbili. 45Hii ilikuwa ndiyo jumla ya wale wa koo za Wamerari. Musa na Haruni waliwahesabu kufuatia amri ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
46Hivyo Musa, Haruni na viongozi wa Israeli waliwahesabu Walawi wote kwa koo zao na jamaa zao. 47Wanaume wote wenye umri wa kuanzia miaka thelathini hadi hamsini waliokuja kufanya kazi ya kuhudumu na kubeba Hema la Kukutania 48walikuwa elfu nane na mia tano themanini (8,580). 49Kwa amri ya Mwenyezi Mungu kupitia Musa, kila mmoja aligawiwa kazi yake na kuambiwa kitu cha kubeba.
Hivyo ndivyo walivyohesabiwa kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia