Walawi 26
26
Thawabu ya utii
(Kumbukumbu 7:12-24; 28:1-14)
1“ ‘Msijitengenezee sanamu, au kusimamisha sanamu ya kuchonga, au jiwe la kuabudia, na pia msijiwekee jiwe lililochongwa katika nchi yenu ili kulisujudia. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
2“ ‘Zishikeni Sabato zangu na kuheshimu mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
3“ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu, 4nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake. 5Kupura nafaka kwenu kutaendelea hadi wakati wa kuvuna zabibu. Na kuvuna zabibu kutaendelea hadi wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.
6“ ‘Nitawapa amani katika nchi, mpate kulala pasipo kutiwa hofu na yeyote. Nitawaondoa wanyama wakali watoke kwenye nchi, nao upanga hautapita katika nchi yenu. 7Mtawafukuza adui zenu, nanyi mtawaua kwa upanga mbele yenu. 8Watu wenu watano watafukuza adui mia moja, na watu wenu mia moja watafukuza adui elfu kumi, nao adui zenu wataanguka kwa upanga mbele yenu.
9“ ‘Nitawaangalia kwa upendeleo na kuwafanya mzae na kuzidisha idadi yenu, nami nitalishika agano langu na ninyi. 10Wakati wa kuvuna mtakuwa bado mnakula mavuno ya mwaka uliopita, na itawalazimu kuyaondoa ghalani ili mpate nafasi ya mavuno mapya. 11Nitafanya makao yangu miongoni mwenu, nami sitawachukia. 12Nitatembea kati yenu niwe Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu. 13Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili msiendelee kuwa watumwa wa Wamisri, nikavunja nira yenu, na kuwawezesha kutembea mkiwa mmeinua vichwa vyenu.
Adhabu ya kutokutii
(Kumbukumbu 28:15-68)
14“ ‘Lakini kama hamtanisikiliza na kutimiza maagizo haya yote, 15nanyi kama mtazikataa amri zangu na kuzichukia sheria zangu, tena mkishindwa kutimiza amri zangu zote, na hivyo mkavunja agano langu, 16ndipo nitakapowafanyia hili: Nitawaletea juu yenu hofu ya ghafula, magonjwa ya kudhoofisha, na homa itakayopofusha macho yenu na kuwaondolea uhai wenu. Mtapanda mbegu bila mafanikio, kwa sababu adui zenu watazila. 17Nitauelekeza uso wangu dhidi yenu ili mshindwe na adui zenu; wale wanaowachukia watawatawala, nanyi mtakimbia ingawa hakuna mtu anayewafukuza.
18“ ‘Kama baada ya haya yote hamtanisikiliza, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu. 19Nitakivunja kiburi chenu cha ukaidi, na kuifanya anga iliyo juu yenu iwe kama chuma, na ardhi yenu kama shaba. 20Nguvu zenu zitatumika bila ya mafanikio, kwa sababu ardhi yenu haitawazalia mazao yake, wala miti ya nchi yenu haitazaa matunda yake.
21“ ‘Kama mtaendelea kuwa na uadui nami, na kukataa kunisikiliza, nitawazidishia mateso yenu mara saba zaidi, kama dhambi zenu zinavyostahili. 22Nitawatuma wanyama mwitu dhidi yenu, nao watawaibieni watoto wenu, watawaangamiza ng’ombe wenu, na kuifanya idadi yenu kuwa ndogo, hivi kwamba barabara zenu zitakuwa hazina watu.
23“ ‘Ikiwa pamoja na mambo haya hamtakubali maonyo yangu lakini mkaendelea kuweka uadui nami, 24mimi mwenyewe nitaweka uadui nanyi, na kuwatesa kwa ajili ya dhambi zenu mara saba zaidi. 25Nitawaletea upanga juu yenu ili kuwapatiliza kwa kuvunja agano langu. Mtakapokimbilia mijini mwenu, nitatuma tauni kati yenu, nanyi mtatiwa mikononi mwa adui zenu. 26Nitakapowaondolea upatikanaji wa mkate wenu, wanawake kumi wataoka mkate wenu katika tanuru moja, nao wataugawa mkate kidogo kwa kupima. Mtakula, lakini hamtashiba.
27“ ‘Kama hata baada ya haya bado hamtanisikiliza lakini mkaendelea kuweka uadui nami, 28ndipo katika hasira yangu nitaweka uadui nanyi, nami mwenyewe nitawaadhibu mara saba kwa ajili ya dhambi zenu. 29Mtakula nyama ya wana wenu na nyama ya binti zenu. 30Nitaharibu mahali penu pa juu pa kuabudia, nibomoe madhabahu yenu ya kufukizia uvumba, na kuzilundika maiti zenu juu ya sanamu zenu zisizo na uhai, nami nitawachukia ninyi. 31Nitaifanya miji yenu kuwa magofu, na kuharibu mahali patakatifu penu pa kuabudia, nami sitapendezwa na harufu nzuri ya sadaka zenu. 32Nitaiharibu nchi, ili adui zenu watakaoishi humo washangae. 33Nitawatawanya ninyi miongoni mwa mataifa, na kuufuta upanga wangu na kuwafuatia. Nchi yenu itaharibiwa, nayo miji yenu itakuwa magofu. 34Ndipo nchi itafurahia sabato zake muda wote ule itakapokuwa ukiwa, nanyi mkiwa katika nchi ya adui zenu. Ndipo nchi itapumzika na kufurahia sabato zake. 35Wakati wote nchi itakapobaki ukiwa, itapumzika na kufurahia sabato zake ambazo haikuzipata mlipokuwa mnaishi humo.
36“ ‘Kwa habari ya wenzenu wale watakaobaki, nitaifanya mioyo yao kuwa na hofu kuu katika nchi za adui zao, kiasi kwamba sauti ya jani linalopeperushwa na upepo itawafanya wakimbie. Watakimbia kana kwamba wanakimbia upanga, nao wataanguka, ijapokuwa hakuna anayewafukuza. 37Watajikwaa mmoja juu ya mwingine kama watu wakimbiao upanga, hata ingawa hakuna anayewafuatia. Hivyo hamtaweza kusimama mbele ya adui zenu. 38Mtaangamia kati ya mataifa; nchi ya adui zenu itawala. 39Wenzenu watakaobaki wataangamia katika nchi za adui zao kwa sababu ya dhambi zao; pia kwa sababu ya dhambi za baba zao wataangamia.
40“ ‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu, 41ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao, 42nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaka, na agano langu na Ibrahimu, nami nitaikumbuka nchi. 43Kwa kuwa wataiacha nchi ukiwa, nayo itafurahia sabato zake wakati itakuwa ukiwa bila wao. Wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao, kwa sababu walizikataa sheria zangu na kuzichukia amri zangu. 44Lakini pamoja na hili, wakati watakuwa katika nchi ya adui zao, sitawakataa wala kuwachukia kiasi cha kuwaangamiza na kuvunja agano langu nao. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao. 45Lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano langu na baba zao, ambao niliwatoa Misri mbele ya mataifa ili niwe Mungu wao. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
46Hizi ndizo amri, sheria na pia masharti ambazo Mwenyezi Mungu alifanya kati yake mwenyewe na Waisraeli katika Mlima Sinai kupitia kwa Musa.
Iliyochaguliwa sasa
Walawi 26: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.