Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 25

25
Mwaka wa Sabato
(Kumbukumbu 15:1-11)
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika Mlima Sinai, 2“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapa ninyi, nchi yenyewe ni lazima ishike sabato kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. 3Kwa miaka sita mtapanda mazao katika mashamba yenu, nanyi kwa miaka sita mtaikata mizabibu yenu matawi na kuvuna mazao yake. 4Lakini katika mwaka wa saba, nchi lazima iwe na sabato ya mapumziko, sabato kwa Mwenyezi Mungu. Msipande mbegu katika mashamba yenu, wala msikate mizabibu yenu matawi. 5Msivune chochote kinachoota chenyewe, wala kuvuna zabibu zenu ambazo hamkuzihudumia. Nchi lazima iwe na mwaka wa mapumziko. 6Chochote nchi itoacho katika mwaka wa sabato kitakuwa chakula chenu wenyewe, watumishi wenu wa kiume na wa kike, mfanyakazi aliyeajiriwa, na mkazi wa muda anayeishi miongoni mwenu, 7vilevile malisho ya mifugo yenu na wanyama pori katika nchi yenu. Chochote nchi itakachozalisha kinaweza kuliwa.
Mwaka wa Yubile
8“ ‘Hesabu sabato saba za miaka saba, yaani miaka saba mara saba, ili sabato saba za miaka saba ziwe muda wa miaka arobaini na tisa. 9Ndipo tarumbeta itapigwa kila mahali katika siku ya kumi ya mwezi wa saba. Katika Siku ya Upatanisho, piga tarumbeta katika nchi yako yote. 10Mwaka wa hamsini mtauweka wakfu na kutangaza uhuru katika nchi kwa wakazi wake wote. Itakuwa ni Yubile#25:10 Yubile ni baragumu iliyopigwa kila mwaka wa hamsini; ni Sabato ya nchi ya kila mwaka wa hamsini uliokuwa mwaka wa ukombozi, yaani kuachia huru. kwenu; kila mmoja wenu atairudia mali ya jamaa yake, na kila mmoja kurudi kwenye ukoo wake. 11Mwaka wa hamsini utakuwa Yubile kwenu, msipande wala msivune kile kinachoota chenyewe, au kuvuna zabibu zisizohudumiwa. 12Kwa kuwa ni Yubile, nayo itakuwa takatifu kwenu; mtakula tu kile kilichotoka moja kwa moja mashambani.
13“ ‘Katika huu Mwaka wa Yubile, kila mmoja atarudi kwenye mali yake mwenyewe.
14“ ‘Ikiwa utauza ardhi kwa mmoja wa wazawa wa nchi yako, au ukinunua ardhi kutoka kwake, mmoja asimpunje mwingine. 15Utanunua ardhi kwa mzawa wa nchi yako kulingana na hesabu ya miaka baada ya Yubile. Naye muuzaji ataiuza kwako kulingana na hesabu ya miaka iliyobaki ya kuvuna mavuno. 16Miaka inapokuwa mingi, utaongeza bei, nayo miaka ikiwa michache, utapunguza bei, kwa sababu kile anachokuuzia kwa hakika ni hesabu ya mazao. 17Mmoja asimpunje mwingine, bali utamcha Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
18“ ‘Fuateni amri zangu na mwe waangalifu kutii amri zangu, nanyi mtaishi salama katika nchi. 19Kisha nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa salama. 20Mwaweza kuuliza, “Tutakula nini katika mwaka wa saba ikiwa hatutapanda wala kuvuna mazao yetu?” 21Nitawaletea baraka ya pekee katika mwaka wa sita, ili nchi iweze kuzalisha mazao ya kuwatosha kwa miaka mitatu. 22Mnapopanda mwaka wa nane, mtakula mavuno ya miaka iliyopita, na mtaendelea kuyala mazao hayo hadi mvune mavuno ya mwaka wa tisa.
23“ ‘Kamwe ardhi isiuzwe kwa mkataba wa kudumu, kwa sababu nchi ni mali yangu, nanyi ni wageni na wapangaji wangu. 24Katika nchi yote mtakayoshika kuwa milki yenu, ni lazima mtoe ukombozi wa ardhi.
25“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini na akauza baadhi ya mali yake, ndugu yake wa karibu atakuja na kukomboa kile ndugu yake alichokiuza. 26Iwapo mtu huyo hana jamaa wa karibu wa kukomboa mali hiyo kwa ajili yake, lakini yeye mwenyewe akafanikiwa na kupata mali itoshayo kuikomboa, 27ataamua tena thamani yake kwa miaka tangu alipoiuza, na kurudisha kiasi kilichobaki cha thamani kwa mtu aliyekuwa amemuuzia mali hiyo, naye ataweza kuirudia mali yake. 28Lakini kama hatapata njia ya kumlipa mnunuzi, ile mali aliyouza itabaki kumilikiwa na mnunuzi hadi Mwaka wa Yubile. Mali hiyo itarudishwa Mwaka wa Yubile, naye ataweza kuirudia mali yake.
29“ ‘Ikiwa mtu atauza nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta, yeye anayo haki ya kuikomboa mwaka mzima baada ya mauzo ya hiyo nyumba. Wakati huo anaweza kuikomboa. 30Ikiwa haikukombolewa kabla ya mwaka mmoja kamili kupita, nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta itakuwa mali ya kudumu ya mnunuzi na wazao wake. Haitarudishwa Mwaka wa Yubile. 31Lakini nyumba zilizo vijijini bila ya kuwa na kuta zilizozizunguka zitahesabiwa kama mashamba. Zinaweza kukombolewa, nazo zirudishwe Mwaka wa Yubile.
32“ ‘Walawi siku zote wana haki ya kukomboa nyumba zao katika miji ya Walawi wanayoimiliki. 33Kwa hiyo mali ya Mlawi inaweza kukombolewa, yaani nyumba iliyouzwa katika mji wowote wanaoushikilia itarudishwa Mwaka wa Yubile, kwa sababu nyumba zilizo katika miji ya Walawi ni mali yao miongoni mwa Waisraeli. 34Lakini maeneo ya malisho yaliyo mali ya miji yao kamwe yasiuzwe, ni milki yao ya kudumu.
35“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe kati yako, msaidie vile ungemsaidia mgeni au mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi kati yako. 36Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi kati yako. 37Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida. 38Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekuleta kutoka nchi ya Misri nikupe nchi ya Kanaani, nami niwe Mungu wako.
39“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini kati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa. 40Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako; naye atatumika hadi Mwaka wa Yubile. 41Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake. 42Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa. 43Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako.
44“ ‘Watumwa wako wa kiume na wa kike watatoka katika mataifa yanayokuzunguka; unaweza kununua watumwa kutoka kwao. 45Pia unaweza kununua baadhi ya wakazi wa muda wanaoishi kati yako, na jamaa ya koo zao waliozaliwa katika nchi yako; nao watakuwa mali yako. 46Unaweza kuwafanya hao kuwa urithi wa watoto wako, na unaweza kuwafanya watumwa kwa maisha yao yote. Lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili.
47“ ‘Ikiwa mgeni au mkazi wa muda katikati yako atakuwa tajiri, na mmoja wa wazawa wa nchi yako akawa maskini, naye akajiuza kwa yule mgeni anayeishi katikati yako, au kwa mmoja wa jamaa wa koo za wageni, 48anayo haki ya kukombolewa baada ya kujiuza. Mmoja wa jamaa zake aweza kumkomboa: 49Mjomba wake, au binamu yake, au yeyote aliye ndugu wa damu katika ukoo wake aweza kumkomboa. Au akifanikiwa, anaweza kujikomboa mwenyewe. 50Yeye na huyo aliyemnunua watahesabu muda kuanzia mwaka aliojiuza hadi Mwaka wa Yubile. Bei ya kuachiwa kwake itakadiriwa kulingana na ujira unaolipwa mfanyakazi wa kuajiriwa kwa idadi ya hiyo miaka. 51Ikiwa imebaki miaka mingi, ni lazima atalipia ukombozi wake fungu kubwa la bei iliyolipwa kumnunua. 52Ikiwa miaka iliyobaki ni michache kufikia Mwaka wa Yubile, atafanya hesabu yake, naye atalipa malipo yanayostahili kwa ajili ya ukombozi wake. 53Atatendewa kama mtu wa kuajiriwa mwaka hadi mwaka; lazima uone kwamba yule aliyemnunua hamtawali kwa ukatili.
54“ ‘Hata ikiwa hakukombolewa kwa njia mojawapo ya hizi, yeye na watoto wake wataachiwa katika Mwaka wa Yubile, 55kwa kuwa kwangu, Waisraeli ni watumishi. Ni watumishi wangu niliowatoa kutoka nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako.

Iliyochaguliwa sasa

Walawi 25: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia