Walawi 24
24
Mafuta na mikate mbele za Mwenyezi Mungu
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Waagize Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili taa ziwe zinawaka daima. 3Nje ya pazia la Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, Haruni ataziwasha taa mbele za Mwenyezi Mungu kuanzia jioni hadi asubuhi daima. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 4Taa zilizo juu ya kinara cha dhahabu safi mbele za Mwenyezi Mungu lazima zihudumiwe daima.
5“Chukua unga laini, uoke mikate kumi na miwili, ukitumia sehemu mbili za kumi ya efa#24:5 Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo mbili. ya unga kwa kila mkate. 6Iweke katika mistari miwili, kila mstari mikate sita, uiweke mbele za Mwenyezi Mungu juu ya meza iliyotengenezwa kwa dhahabu safi. 7Kando ya kila mstari, weka uvumba safi kama sehemu ya kumbukumbu ili kuwakilisha mikate kuwa sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto. 8Mikate hii itawekwa mbele za Mwenyezi Mungu kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa agano la kudumu. 9Hii ni mali ya Haruni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao milele la sadaka iliyotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuteketezwa kwa moto.”
Mwenye kukufuru apigwa mawe
10Basi mwana wa mama Mwisraeli na baba Mmisri alienda miongoni mwa Waisraeli, nayo mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli. 11Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru Jina la Mwenyezi Mungu kwa kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Musa. (Mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri, wa kabila la Dani.) 12Nao wakamweka mahabusu hadi mapenzi ya Mwenyezi Mungu yawe wazi kwao.
13Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: 14“Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote watampiga mawe. 15Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake. 16Yeyote atakayekufuru Jina la Mwenyezi Mungu ni lazima auawe. Kusanyiko lote watampiga kwa mawe. Iwe ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la Mwenyezi Mungu, ni lazima auawe.
17“ ‘Kama mtu yeyote atamuua mtu mwingine, ni lazima auawe. 18Mtu yeyote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai. 19Ikiwa mtu yeyote atamjeruhi jirani yake, chochote alichomtenda naye atatendewa: 20iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa. 21Yeyote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini yeyote auaye mtu, lazima auawe. 22Mtakuwa na sheria hiyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”
23Kisha Musa akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
Iliyochaguliwa sasa
Walawi 24: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.