Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 22

22
Elifazi anasema: Uovu wa Ayubu ni mkubwa
1Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
2“Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu?
Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?
3Je, Mwenyezi angefurahia nini
kama ungekuwa mwadilifu?
Au je, yeye angepata faida gani
kama njia zako zingekuwa kamilifu?
4“Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea
na kuleta mashtaka dhidi yako?
5Je, uovu wako si mkuu?
Dhambi zako si hazina mwisho?
6Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu;
umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.
7Hukumpa maji aliyechoka,
nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,
8ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi:
mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.
9Umewafukuza wajane mikono mitupu
na kuzivunja nguvu za yatima.
10Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote,
hatari ya ghafula inakutia hofu,
11ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona,
tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.
12“Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu?
Juu kuliko nyota zilizo juu sana!
13Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’
Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?
14Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi
atembeapo juu ya anga la dunia.
15Je, utaifuata njia ya zamani,
ambayo watu waovu waliikanyaga?
16Waliondolewa kabla ya wakati wao,
misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.
17Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi!
Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’
18Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri,
hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.
19“Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi,
nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,
20‘Hakika adui zetu wameangamizwa,
nao moto umeteketeza mali yao.’
21“Mjue sana Mungu ili uwe na amani,
ndipo mema yatakapokujia.
22Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake,
na maneno yake uyaweke moyoni mwako.
23Ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya:
Ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,
24kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi,
dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,
25ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako,
naye atakuwa fedha yako iliyo bora.
26Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi,
nawe utamwinulia Mungu uso wako.
27Utamwomba yeye, naye atakusikia,
nawe utazitimiza nadhiri zako.
28Utakusudia jambo nalo litatendeka,
nao mwanga utaangazia njia zako.
29Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’
ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.
30Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia,
ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia