Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 21

21
Hotuba ya saba ya Ayubu
Ayubu anajibu: Waovu mara nyingi huenda bila kuadhibiwa
1Ndipo Ayubu akajibu:
2“Yasikilizeni maneno yangu kwa makini;
hii na iwe faraja mnayonipa mimi.
3Nivumilieni ninapozungumza,
nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.
4“Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu?
Kwa nini nisikose subira?
5Niangalieni mkastaajabu;
mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.
6Ninapowaza kuhusu hili, ninaogopa,
nao mwili wangu unatetemeka.
7Kwa nini waovu wanaendelea kuishi,
wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?
8Huwaona watoto wao wakithibitika
wakiwa wamewazunguka,
wazao wao mbele za macho yao.
9Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu;
fimbo ya Mungu haiko juu yao.
10Madume yao ya ng’ombe huvyaza bila kushindwa kamwe;
ng’ombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.
11Huwatoa watoto wao nje kama kundi;
wadogo wao huchezacheza.
12Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi,
nao huifurahia sauti ya filimbi.
13Huitumia miaka yao katika mafanikio
nao hushuka kaburini kwa amani.
14Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’
Hatuna haja ya kufahamu njia zako.
15Mwenyezi ni nani hata tumtumikie?
Tutapata faida gani kumwomba?
16Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe,
hivyo najitenga mbali na ushauri wa waovu.
17“Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa?
Ni mara ngapi maafa huwajia,
yale yawapatayo ambayo Mungu
huwapangia katika hasira yake?
18Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo,
kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?
19Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu
kwa ajili ya wanawe.’
Mungu na amlipe mtu mwenyewe,
ili apate kulijua!
20Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake;
yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.
21Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma,
miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?
22“Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,
iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?
23Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili,
akiwa salama na mwenye amani,
24mwili wake ukiwa umenawiri,
nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta.
25Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi,
akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.
26Hao wote hulala mavumbini,
nao mabuu huwafunika wote.
27“Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri,
mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.
28Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu,
mahema ambayo watu waovu walikaa?’
29Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri?
Je, hamkutafakari taarifa zao:
30kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa,
kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?
31Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake?
Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?
32Hupelekwa kaburini,
nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.
33Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake;
watu wote watamfuata,
nao umati wa watu wasiohesabika wamemtangulia.
34“Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu?
Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia