Ayubu 23
23
Hotuba ya nane ya Ayubu
Ayubu anajibu: Nalalamika kwa uchungu
1Ndipo Ayubu akajibu:
2“Hata leo malalamiko yangu ni ya uchungu;
mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.
3Laiti ningefahamu mahali pa kumwona;
laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!
4Ningeleta kesi yangu mbele zake,
na kukijaza kinywa changu na hoja.
5Ningejua kwamba angenijibu nini,
na kuelewa lile angeniambia.
6Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?
La, hangenigandamiza.
7Hapo mtu mwadilifu angeleta kesi yake mbele zake,
nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.
8“Lakini nikienda mashariki, hayupo;
nikienda magharibi, simpati.
9Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni;
akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.
10Lakini anaijua njia niiendeayo;
akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu;
nimeishika njia yake bila kukengeuka.
12Sijaziacha amri zilizotoka mdomoni mwake;
nimeyathamini maneno ya kinywa chake
kuliko chakula changu cha kila siku.
13“Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga?
Yeye hufanya lolote atakalo.
14Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,
na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.
15Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake;
nifikiriapo haya yote ninamwogopa.
16Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia;
yeye Mwenyezi amenitia hofu.
17Hata hivyo sijanyamazishwa na giza,
wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.