Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 29

29
Ole wa Mji wa Daudi
1Ole wako, wewe Arieli, Arieli,
mji alimokaa Daudi!
Ongezeni mwaka kwa mwaka,
na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.
2Hata hivyo nitauzingira Arieli kwa jeshi,
utalia na kuomboleza,
utakuwa kwangu kama mahali
pa kuwashia moto madhabahuni.
3Nitapiga kambi pande zote dhidi yako,
nitakuzunguka kwa minara
na kujenga ngome yakukuzingira.
4Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini,
utamumunya maneno yako kutoka mavumbini.
Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu,
utanong’ona maneno yako toka mavumbini.
5Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini;
makundi ya watu wakatili watakuwa
kama makapi yanayopeperushwa.
Naam, ghafula, mara moja,
6Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atakuja
na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu,
atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.
7Kisha makundi ya mataifa yote yanayopigana dhidi ya Arieli,
yale yanayomshambulia yeye na ngome zake,
na kumzingira kwa jeshi,
watakuwa kama ilivyo ndoto,
kama maono wakati wa usiku:
8kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula,
lakini huamka, bado njaa yake ingalipo,
kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji,
lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu.
Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa
yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.
9Pigweni na butwaa na mshangae;
jifanyeni vipofu wenyewe na msione;
leweni, lakini si kwa mvinyo,
pepesukeni lakini si kwa kileo.
10Mwenyezi Mungu amewaleteeni usingizi mzito:
Ameziba macho yenu ninyi manabii;
amefunika vichwa vyenu ninyi waonaji.
11Kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa muhuri katika kitabu. Mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri.” 12Au mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”
13Bwana asema:
“Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao
na kuniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
Ibada yao kwangu inatokana na maagizo
waliyofundishwa na wanadamu.
14Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,
kwa ajabu juu ya ajabu.
Hekima ya wenye hekima itapotea,
nayo akili ya wenye akili itatoweka.”
15Ole kwa wale wanaoenda kwenye vilindi virefu
kumficha Mwenyezi Mungu mipango yao,
wafanyao kazi zao gizani na kufikiri,
“Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”
16Mnapindua mambo juu chini,
kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi!
Je, kile kilichofinyangwa
chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga,
“Wewe hukunifinyanga mimi”?
Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi,
“Wewe hujui chochote”?
17Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa
kuwa shamba lenye rutuba,
na shamba lenye rutuba
liwe kama msitu?
18Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu,
na katika utusitusi na giza
macho ya kipofu yataona.
19Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Mwenyezi Mungu,
wahitaji watafurahi ndani yake Aliye Mtakatifu wa Israeli.
20Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea,
nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,
21wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia,
wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama,
na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki
yeye asiye na hatia.
22Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, aliyemkomboa Ibrahimu, analosema kwa nyumba ya Yakobo:
“Yakobo hataaibishwa tena,
wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.
23Watakapoona watoto wao miongoni mwao,
kazi ya mikono yangu,
watalitakasa Jina langu takatifu;
wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo,
nao watamcha Mungu wa Israeli.
24Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu,
nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 29: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia