Isaya 30
30
Ole wa taifa kaidi
1Mwenyezi Mungu asema,
“Ole kwa watoto wakaidi,
kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu,
wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu Mtakatifu,
wakilundika dhambi juu ya dhambi,
2wale wanaoshuka kwenda Misri
bila kutaka ushauri wangu,
wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao,
wanaotafuta kivuli cha Misri kiwe kimbilio.
3Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu,
kivuli cha Misri kitawaletea fedheha.
4Ingawa wana maafisa katika Soani
na wajumbe wamewasili katika Hanesi,
5kila mmoja ataaibishwa
kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu,
ambalo haliwaletei msaada wala faida,
bali aibu tu na fedheha.”
6Neno la unabii kuhusu wanyama wa Negebu:
Katika nchi ya taabu na shida,
ya simba za dume na jike,
ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao,
wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda,
hazina zao juu ya nundu za ngamia,
kwa lile taifa lisilokuwa na faida,
7kuvipeleka Misri,
ambaye msaada wake haufai kabisa.
Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.”
8Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao,
liandike kwenye kitabu,
ili liweze kuwa shahidi milele
kwa ajili ya siku zijazo.
9Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu,
watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
10Wanawaambia waonaji,
“Msione maono tena!”
Nako kwa manabii wanasema,
“Msiendelee kutupatia maono
ambayo ni ya kweli!
Tuambieni mambo ya kupendeza,
tabirini mambo ya uongo.
11Acheni njia hii,
ondokeni katika mapito haya,
nanyi acheni kutukabili pamoja
na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!”
12Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Kwa sababu mmekataa ujumbe huu,
mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu,
13dhambi hii itakuwa kwenu
kama ukuta mrefu,
wenye ufa na wenye kubetuka,
ambao unaanguka ghafula,
mara moja.
14Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo
ukipasuka pasipo huruma
ambapo katika vipande vyake
hakuna kipande kitakachopatikana
kwa kuukulia makaa kutoka jikoni
au kuchotea maji kisimani.”
15Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo:
“Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu,
katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu,
lakini hamkutaka.
16Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’
Kwa hiyo mtakimbia!
Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi wanaoenda kasi.’
Kwa hiyo wanaowafukuza wataenda kasi!
17Watu elfu moja watakimbia
kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja,
kwa vitishio vya watu watano
wote mtakimbia,
hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera
juu ya kilele cha mlima,
kama bendera juu ya kilima.”
18Hata hivyo Mwenyezi Mungu anatamani kutupatia neema,
anainuka ili kuwaonesha huruma.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa haki.
Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!
19Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. 20Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. 21Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” 22Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!”
23Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ng’ombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. 24Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. 25Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. 26Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utang’aa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati Mwenyezi Mungu atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.
27Tazama, Jina la Mwenyezi Mungu linakuja kutoka mbali,
likiwa na hasira kali inayowaka
pamoja na wingu zito la moshi,
midomo yake imejaa ghadhabu
na ulimi wake ni moto ulao.
28Pumzi yake ni kama mkondo wa maji yaendayo kasi,
yakipanda hadi shingoni.
Hutikisa mataifa katika chujio ya uharibifu,
huweka lijamu katika mataya ya mataifa
ambayo huwaongoza upotevuni.
29Nanyi mtaimba kama usiku ule mnaadhimisha
sikukuu takatifu.
Mioyo yenu itashangilia
kama vile watu wanapokwea na filimbi
kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu,
kwa Mwamba wa Israeli.
30Mwenyezi Mungu atawasababisha watu waisikie sauti yake ya utukufu,
naye atawafanya wauone mkono wake ukishuka
pamoja na hasira yake kali na moto ulao,
kukiwa na tufani ya mvua,
ngurumo za radi na mvua ya mawe.
31Sauti ya Mwenyezi Mungu itaivunjavunja Ashuru,
kwa fimbo yake ya utawala atawapiga.
32Kila pigo Mwenyezi Mungu atakaloliweka juu yao
kwa fimbo yake ya kuadhibu,
litakuwa kwa wimbo wa matari na vinubi,
anapopigana nao katika vita
kwa mapigo ya mkono wake.
33Tofethi pameandaliwa toka zamani,
pamewekwa tayari kwa ajili ya mfalme.
Shimo lake la moto limetengenezwa kwa kina kirefu
na kwa upana mkubwa,
likiwa na moto na kuni tele;
pumzi ya Mwenyezi Mungu,
kama kijito cha kiberiti,
huuwasha moto.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 30: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.