Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 28

28
Ole wa Efraimu
1Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu,
kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,
uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba:
kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!
2Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu.
Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo unaoharibu,
kama mvua inayonyesha kwa nguvu na mafuriko yanayoshuka,
atakiangusha chini kwa nguvu.
3Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu,
kitakanyagwa chini ya nyayo.
4Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,
uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba,
litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno:
mara mtu aionapo, huichuma na kuila.
5Katika siku ile, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
atakuwa taji la utukufu,
taji zuri la maua
kwa mabaki ya watu wake.
6Atakuwa roho ya haki
kwa yeye anayeketi kwenye kiti cha hukumu,
chanzo cha nguvu
kwa wale wazuiao vita langoni.
7Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo,
wanayumbayumba kwa sababu ya kileo:
Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo,
wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo;
wanapepesuka wanapoona maono,
wanajikwaa wanapotoa maamuzi.
8Meza zote zimejawa na matapishi
wala hakuna sehemu hata ndogo
isiyokuwa na uchafu.
9“Yeye anajaribu kumfundisha nani?
Yeye anamwelezea nani ujumbe wake?
Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya?
Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?
10Kwa maana ni:
Amri juu ya amri, amri juu ya amri,
kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni;
hapa kidogo, kule kidogo.”
11Sawa kabisa, kwa midomo migeni
na kwa lugha ngeni,
Mungu atasema na watu hawa,
12wale ambao aliwaambia,
“Hapa ni mahali pa kupumzika,
waliochoka na wapumzike,”
na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,”
lakini hawakutaka kusikiliza.
13Hivyo basi, neno la Mwenyezi Mungu kwao litakuwa:
Amri juu ya amri, amri juu ya amri,
kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni,
hapa kidogo, kule kidogo:
ili waende na kuanguka chali,
wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.
14Kwa hiyo sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wenye dharau
mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.
15Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti,
tumefanya mapatano na Kuzimu#28:15 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho..
Pigo linalofurika litakapopita,
haliwezi kutugusa sisi,
kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu
na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”
16Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni,
jiwe lililojaribiwa,
jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti.
Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu.
17Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia
na uadilifu kuwa timazi;
mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo,
nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha.
18Agano lenu na kifo litabatilishwa,
patano lenu na Kuzimu halitasimama.
Pigo linalofurika litakapowakumba,
litawaangusha chini.
19Kila mara lijapo litawachukua,
asubuhi baada ya asubuhi,
wakati wa mchana na wakati wa usiku,
litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.”
Kuuelewa ujumbe huu
utaleta hofu tupu.
20Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake,
nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno
mtu hawezi kujifunikia.
21Mwenyezi Mungu atainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu,
ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni:
ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu,
ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni.
22Sasa acheni dharau zenu,
la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi.
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ameniambia
habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote.
23Sikilizeni msikie sauti yangu,
tegeni masikio na msikie niyasemayo.
24Mkulima anapolima ili apande,
je, hulima siku zote?
Je, huendelea kubomoa ardhi
na kusawazisha udongo?
25Baada ya kusawazisha shamba,
je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira?
Je, hapandi ngano katika sehemu yake,
shayiri katika eneo lake,
na nafaka nyingine katika shamba lake?
26Mungu wake humwelekeza
na kumfundisha njia iliyo sahihi.
27Iliki haipurwi kwa nyundo,
wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira;
iliki hupurwa kwa fimbo,
na jira kwa ufito.
28Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate,
kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima.
Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake,
farasi wake hawasagi.
29Haya yote pia hutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 28: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia