1 Samweli 16:11-23
1 Samweli 16:11-23 NENO
Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.” Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.” Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Aling’aa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.” Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama. Basi Roho wa Mwenyezi Mungu alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu ili imtese. Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na Mwenyezi Mungu nayo inakutesa. Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.” Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.” Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Mwenyezi Mungu yu pamoja naye.” Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe. Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake. Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.” Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.