1 Sam 16:11-23
1 Sam 16:11-23 SUV
Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee. Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.